Numbers 32

Makabila Ng’ambo Ya Yordani

(Kumbukumbu 3:12-22)

1 aKabila la Wareubeni na Wagadi, waliokuwa na makundi makubwa ya ng’ombe, kondoo na mbuzi, waliona kuwa nchi ya Yazeri na nchi ya Gileadi ni nzuri kwa mifugo. 2 bHivyo walimjia Musa, na kuhani Eleazari na viongozi wa jumuiya, na kuwaambia, 3 c“Atarothi, Diboni, Yazeri, Nimra, Heshboni, Eleale, Sebamu, Nebo na Beoni, 4 dnchi ambayo Bwana ameishinda mbele ya wana wa Israeli, inafaa kwa mifugo, nao watumishi wako wana mifugo. 5 eKama tumepata kibali mbele ya macho yako, nchi hii na ipewe watumishi wako kama milki yetu. Usitufanye tuvuke Yordani.”

6Musa akawaambia Wagadi na Wareubeni, “Je, watu wa nchi yenu watakwenda vitani wakati ninyi mmeketi hapa? 7 fKwa nini mmewakatisha Waisraeli tamaa wasivuke katika nchi ambayo Bwana amewapa? 8 gHivi ndivyo baba zenu walivyofanya wakati nilipowatuma kutoka Kadesh-Barnea kuipeleleza nchi. 9 hBaada ya kufika kwenye Bonde la Eshkoli na kuitazama nchi, waliwakatisha tamaa Waisraeli wasiingie katika nchi ambayo Bwana alikuwa amewapa. 10 iSiku ile hasira ya Bwana iliwaka naye akaapa kiapo hiki: 11 j‘Kwa kuwa hawakunifuata kwa moyo wote, hakuna mtu yeyote mwenye miaka ishirini au zaidi ambaye alikuja kutoka Misri atakayeona nchi niliyoahidi kwa kiapo kwa Ibrahimu, Isaka na Yakobo; 12 khakuna hata mmoja isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni, kwa sababu walimfuata Bwana kwa moyo wote.’ 13 lHasira ya Bwana iliwaka dhidi ya Waisraeli na akawafanya watangetange katika jangwa kwa miaka arobaini, mpaka kizazi chote cha wale waliofanya maovu mbele yake kimeangamia.

14 m“Nanyi mko hapa, uzao wa wenye dhambi, mkisimamia mahali pa baba zenu na mkimfanya Bwana kuwakasirikia Waisraeli hata zaidi. 15 nKama mkigeuka na mkiacha kumfuata, atawaacha tena watu hawa wote jangwani, na mtakuwa sababu ya maangamizi yao.”

16 oNdipo wakamjia Musa na kumwambia, “Tungalitaka kujenga mazizi hapa kwa ajili ya mifugo yetu na miji kwa ajili ya wanawake wetu na watoto. 17 pLakini sisi tuko tayari kuchukua silaha zetu na kutangulia mbele ya Waisraeli mpaka tutakapowaleta mahali pao. Wakati huo wanawake wetu na watoto wataishi katika miji yenye ngome, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya wenyeji wa nchi. 18 qHatutarudi nyumbani mwetu mpaka kila Mwisraeli apokee urithi wake. 19 rHatutapokea urithi wowote pamoja nao ng’ambo ya Yordani, kwa sababu urithi wetu umekuja kwetu upande wa mashariki ya Yordani.”

20 sKisha Musa akawaambia, “Kama mtafanya jambo hili, kama mtajivika silaha mbele za Bwana kwa ajili ya vita, 21na kama ninyi nyote mtakwenda mmejivika silaha ng’ambo ya Yordani mbele za Bwana mpaka awe amewafukuza adui zake mbele zake, 22 thadi wakati nchi itakapokuwa imeshindwa mbele za Bwana, ndipo mtaweza kurudi na kuwa huru kutoka masharti yenu kwa Bwana na Israeli. Nayo nchi hii itakuwa milki yenu mbele za Bwana.

23 u“Lakini mkishindwa kufanya hili, mtakuwa mnatenda dhambi dhidi ya Bwana; nanyi kuweni na hakika kuwa dhambi yenu itawapata. 24 vJengeni miji kwa ajili ya wanawake na watoto wenu, na mazizi kwa ajili ya mbuzi na kondoo zenu, lakini fanyeni yale mliyoahidi.”

25 wWagadi na Wareubeni wakamwambia Musa, “Sisi watumishi wako tutafanya kama bwana wetu anavyotuagiza. 26 xWatoto na wake zetu, makundi ya mbuzi na kondoo, na makundi ya ng’ombe zetu, watabaki hapa katika miji ya Gileadi. 27 yLakini watumishi wenu, kila mwanaume aliyevaa silaha za vita, watavuka ng’ambo kupigana mbele za Bwana, sawa kama bwana wetu anavyosema.”

28 zKisha Musa akatoa amri kuhusu wao kwa kuhani Eleazari, na Yoshua mwana wa Nuni na viongozi wa jamaa za makabila ya Waisraeli. 29 aaMusa akawaambia, “Ikiwa Wagadi na Wareubeni, kila mwanaume aliyevaa silaha za vita, atavuka Yordani pamoja nanyi mbele za Bwana, basi wakati mtakapoishinda nchi iliyoko mbele yenu, wapeni nchi ya Gileadi kama milki yao. 30Lakini kama hawatavuka pamoja nanyi wakiwa wamevaa silaha za vita, lazima wakubali kupokea milki yao pamoja nanyi katika nchi ya Kanaani.”

31Wagadi na Wareubeni wakajibu, “Watumishi wako watafanya lile Bwana alilosema. 32 abTutavuka mbele za Bwana kuingia Kanaani tukiwa tumevaa silaha za vita, lakini mali tutakayoirithi itakuwa ng’ambo hii ya Yordani.”

33 acKisha Musa akawapa Wagadi, Wareubeni, na nusu ya kabila la Manase mwana wa Yusufu ufalme wa Sihoni mfalme wa Waamori, na ufalme wa Ogu mfalme wa Bashani, nchi yote pamoja na miji yake, na nchi inayowazunguka.

34 adWagadi wakajenga Diboni, Atarothi, Aroeri, 35 aeAtroth-Shofani, Yazeri, Yogbeha, 36Beth-Nimra na Beth-Harani kama miji iliyozungushiwa ngome, tena wakajenga mazizi kwa ajili ya makundi yao ya mbuzi na kondoo. 37 afNao Wareubeni wakajenga upya miji ya Heshboni, Eleale na Kiriathaimu, 38 agpia Nebo na Baal-Meoni (majina ya hiyo miji yalibadilishwa) na Sibma. Miji waliyoijenga upya waliipa majina.

39 ahWazao wa Makiri mwana wa Manase walikwenda Gileadi, wakaiteka nchi na kuwafukuza Waamori waliokuwa huko. 40 aiKwa hiyo Musa akawapa Wamakiri, wazao wa Manase, nchi ya Gileadi, nao wakakaa huko. 41 ajYairi, mzao wa Manase, akateka makao yao, akayaita Hawoth-Yairi. 42 akNaye Noba akateka Kenathi na makao yaliyoizunguka, akayaita Noba kwa jina lake.
Copyright information for SwhKC